Home » » KANYIGO WAKUSUDIA KUKUSANYA FEDHA ZA KUKUZA ELIMU

KANYIGO WAKUSUDIA KUKUSANYA FEDHA ZA KUKUZA ELIMU

Na Mwandishi Wetu, Kagera
UMOJA wa Maendeleo ya Kanyigo mkoani Kagera (KADEA), umedhamiria kukusanya Sh milioni 90 kila mwaka, kwa ajili ya kukuza maendeleo ya elimu kwa kujenga shule.

Akizungumza mjini hapa jana, Mweka Hazina wa Umoja huo, Moses Kagya, alisema fedha zote zitakazopatikana zitaelekezwa katika miradi mbalimbali ya elimu ya Kata ya Kanyigo.

“Nawahakikishia wana Kanyigo wote kwamba michango watakayotoa itakuwa salama na itakwenda kuendeleza elimu na uongozi umekuwa na uadilifu na utaendelea kuwa na uadilifu mkubwa.

“Tunawaomba wana Kanyigo popote walipo ndani na nje ya nchi, wachangie kwa hali na mali umoja huu kwa maendeleo ya kata na Taifa letu kwa ujumla, tumedhamiria kuipaisha kata yetu kielimu na tunataka iwe mfano wa kuigwa,” alisema Kagya.

Aliwaomba wenye mchango kuweka katika akaunti za umoja huo za 01J2055691900 CRDB na 3186600382 NMB.

Kuhusu maazimio ya semina iliyojumuisha wenyeviti wa vitongoji na vijiji, viongozi wa dini, viongozi wa kata, viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi, viongozi wa saccis na uongozi wa juu wa KADEA, alisema wameazimia kuiomba kila kaya katika kata zao mbili kuchangia si chini ya Sh 5,000 kila ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Alisema wana Kanyigo waishio nje ya Kanyigo wakiwamo wa nje ya nchi wameombwa kuchangia si chini ya Sh 20,000 kila mmoja ifikapo mwisho wa mwaka.

Alisema kurejesha heshima ya Kanyigo katika ulimwengu wa elimu wameamua kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Kanyigo ambao kwa kuanzia utalenga kuinua elimu ya msingi.

Alisema lengo ni kuwezesha wanafunzi wasiopungua 400 kuchaguliwa kwenda sekondari kila mwaka kuanzia mwakani tofauti na sasa ambapo wanaochaguliwa ni 200.

“Hawa ndio wanaopata daraja la nne na 0 katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne, kwa kifupi tumeamua kufanya mambo mengi kufanikisha mfuko huu na kuinua kiwango cha elimu Kanyigo,” alisema Kagya.

Alisema semina ilifanyika sekondari ya Kanyigo Julai 7, mwaka huu na maazimio yaliwasilishwa katika mikutano ya vitongoji na vijiji na vikao vya maendeleo ya kata na kuafikiwa.

Alisema mada kuu ya semina ilikuwa ni kutafuta mbinu za kuboresha elimu katika kata zao mbili kwa kuwa hali ya elimu si ya kuridhisha.

“Tunazo shule za msingi 12, kati ya hizo ni moja tu inayofanya vizuri ambayo ni Josiah Kibira English Medium. Tunazo shule za sekondari tano, lakini kati ya hizo ni moja inayofanya vizuri ambayo ni Kanyigo Secondary School,” alisema Kagya.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa