Na Arodia Peter
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, ameiasa Serikali ya Tanzania kutojaribu kuingia vitani kupigana na Malawi, kutokana na mzozo wa mipaka unaoendelea.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Askofu Kilaini alisema njia pekee ambayo inaweza kuleta suluhu ni mazungumzo baina ya pande zote mbili.
“Nimesikia kauli za viongozi wetu, nimeshtuka mno… sipendi kuona taifa letu linaingia kwenye vita wakati huu, wote tunakumbuka mwaka 1978, wakati tulipopigana na Uganda,
….ile vita ilitusababisha Watanzania tufunge mkanda wakati wote, makovu yake bado yanaonekana, namuomba Mungu aepushe jambo hili,” alisema Askofu Kilaini.
Alisema umefika wakati wa Serikali ya Tanzania na Malawi, kukutana kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi, kuliko kuendeleza vitisho ambavyo vinaweza kuleta athari kubwa kwa pande zote.
“Nimesikitika kuona viongozi wa Tanzania, wanahamaki kuhusu mgogoro huo…zitumike mbinu za kidiplomasia kufikia muafaka, ili wananchi wa pande zote waendelee na jitihada za kujiondelea umasikini unaowakabili,” alisema Askofu Kilaini.
Alisema pamoja na kushauri pande hizo, zikutane aliitaka Tanzania kutokubali kunyang’anywa ardhi inayomiliki kihalali.
“Viongozi wetu naona wanatoa matamko kila siku, wenzao wamekaa kimya, jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa.
“Tukumbuke kauli aliyowahi kuitoa Rais wa zamani wa Malawi, Kamuzu Banda, kwamba Watanzania ni mabingwa wa maneno, lakini Wamalawi ni watu wa vitendo.
“Hatutaki kugombana, twende katika mazungumzo, tutumie njia za kidiplomasia kutatua mgogoro huu, lakini Tanzania isibweteke kwa ukimya wa Malawi,” alisema Askofu Kilaini.
Mgogoro wa Tanzania na Malawi ni wa siku nyingi na chanzo chake ni mpaka ndani ya Ziwa Nyasa.
Kwa muda sasa, Malawi inadai eneo lote kaskazini ya Msumbiji kuelekea mikoa ya Ruvuma na Mbeya ni mali yao, hii ni kwa mujibu wa mkataba wa Heligoland uliosainiwa Julai, 1890.
Lakini Tanzania kwa upande wake, inadai mpaka kati ya nchi hizo, unapita katikati ya ziwa hilo, usawa wa nyuzi 11 Kusini hadi mwisho wa ziwa katika eneo la Kyera.
Tanzania inadai nyaraka za ramani zilizotengenezwa na wakoloni Waingereza mwaka 1928, 1937 na 1939, zote zinaonyesha mpaka wa ziwa hilo upo katikati ya Ziwa Nyasa.
Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa aliwaambia waandishi wa habari kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), liko tayari kukabiliana na tishio lolote kwa ajili ya kuwalinda Watanzania pamoja na mipaka yake.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment