Home » » MNYAUKO WA MIGOMBA WAANZA KUZUA BALAA KAGERA

MNYAUKO WA MIGOMBA WAANZA KUZUA BALAA KAGERA


Na Audax Mutiganzi, Bukoba
UGONJWA wa mnyauko unaoshambulia migomba umeanza kuathiri upatikanaji wa ndizi katika maeneo mbalimbali mkoani Kagera.

Ugonjwa huo ambao hadi sasa haujajulikana unasababishwa na nini, unasambaa kwa kasi, hasa katika maeneo ya wilaya za Muleba na Karagwe, Misenyi na Bukoba ambazo zimekuwa zikizalisha ndizi kwa wingi mkoani Kagera.

Ugonjwa huo umesababisha kupungua kwa uzalishaji wa ndizi mkoani hapa, jambo ambalo limechangia kupanda kwa bei ya ndizi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba katika soko kuu la Bukoba ndizi kubwa zinauzwa kwa wastani wa kati ya Sh 15, 000 hadi 20, 000 ambapo miaka iliyopita ndizi hizo ziliuzwa kwa kati ya Sh 6,000 hadi 8,000.

Kupanda kwa bei ya ndizi iliyochangiwa na ugonjwa wa mnyauko wa migomba kumewalazimisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kagera ambao hutegemea ndizi kama chakula chao kikuu kubadilika na sasa wanalazimika kula ugali na wali.

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera wamelazimika kubadili fikira zao za kudhani kuwa ndizi ndicho chakula kikuu baada ya kushindwa kumudu gharama za kununua ndizi katika masoko kutokana na bei yake kuwa kubwa.

Baadhi ya wakulima bora wa migomba mkoani hapa ambao mashamba yao yameathirika kutokana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba ni pamoja na Kamishina Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Alfred Tibaigana.

Kamishina Tibaigana shamba lake lililoko katika kijiji cha Buganguzi wilayani Muleba limeathirika sana. Mkulima huyu kabla ya ugonjwa huu alikuwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 40 za ndizi kwa wiki, ambapo sasa anazalisha wastani wa tani zisizozidi 10 kwa wiki.

Baadhi ya wakulima mkoani Kagera wameitahadharisha serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi, ili zao la ndizi lisibaki katika vitabu vya historia.

Kwa upande wake Sai Bulili, mtafiti wa Kituo cha Mazao cha Maruku kilichoko katika Wilaya ya Bukoba vijijini, alisema ugonjwa wa mnyauko hadi sasa bado haujapata tiba.

Bulili alisema wakulima ili waweze kuepukana na ugonjwa huo ni lazima wafuate tararibu zote za kupambana na ugonjwa huo wanazoelekezwa na wataalamu wa kilimo, ambazo ni pamoja na kuing'oa na kuichoma moto miche yote ya migomba inayoonyesha dalili za ugonjwa huo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa