na Ashura Jumapili, Muleba
WANANCHI wa Kata ya Rutoro jimbo la Muleba Kaskazini mkoani Kagera, wamesema matatizo ya ardhi yanayowakumba yanasababishwa na siasa za Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kauli hiyo ilitolewa kwa nyakati tofauti na wananchi hao walipokuwa wakizungumza na Tanzania Daima juzi, juu ya migogoro inayotokea mara kwa mara eneo hilo kati ya wakulima na wafugaji.
Walibainisha, kwa muda wa miaka saba wakulima na wafugaji wamekuwa na ugomvi, lakini hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Profesa Anna Tibaijuka alisema ameumaliza mgogoro huo.
Waliongeza kuwa Waziri Tibaijuka aliwataka wakulima waendelee kulima bila kutoa uthibitisho wa kumaliza mgogoro huo.
Bartazari Kihanga, mkazi wa Kitongoji cha Rwamtukuza kijiji Buyeke, kata ya Rutoro, alisema hajui njia iliyotumiwa na Waziri Tibaijuka kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda wa miaka saba ikihusisha wafugaji na wakulima.
Kihanga alisema katika kikao cha waziri huyo na wanachi hao, hakueleza wenye haki ya kumiliki eneo linalogombewa ni kina nani baina ya wakulima na wafugaji ambao ni Wanyarwanda wenye uraia wa Tanzania waliovamia eneo hilo mwaka 2006 na kujiita wawekezaji.
Francis Tibahika mkazi wa kitongoji Charutale, alisema maneno ya waziri ni siasa za Chama cha Mapinduzi kama ameumaliza mgogoro huu angetuachia kibali kwani yeye ni waziri anayehusika na mgogoro huu kwa maana ya wizara yake.
Alisema, baada ya Waziri Tibaijuka kuondoka wafugaji hao walipeleka ng’ombe kwenye mashamba ya wakulima jambo lililofanya mazao yaliyokuwapo yaharibike sambamba na kuchochea kutoelewana kwa pande hizo mbili.
Athuman Ruhazi alisema wananchi wa kata hiyo wana hali ngumu ya kimaisha kwani mashmba waliyoyategemea kwa ajili ya mazao ya chakula na biashara sasa yamegeuzwa sehemu ya malisho ya mifugo.
Ruhazi alisema kumekuwa na madai kutoka kwa Wanyarwanda hao kuwa wanataka kuokomboa mkoa wa Kagera ili kuunganisha na nchi yao ya Rwanda.
Aliongeza kuwa taarifa za madai hayo walishazitoa kwa viongozi wa serikali ya Tanzania lakini mpaka sasa hakuna hatua yoyote iliyochukulia dhidi ya kauli hizo.
Naye kwa upande wake diwani wa kata ya Rutoro, Abubakar Bushumbiro, alisema mgogoro wa ardhi umesababisha wanawake kubakwa, wananchi kujeruhiwa na wafugaji.
Bushumbiro alisema wafugaji hao wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa wananchi kwa kuwabaka wakiwa njiani au kuwavamia majumbani mwao.
Alisema kuna wananchi wawili waliokatwa masikio na wafugaji hao ambao ni Modest Kiraja na mwenyekiti wa kitongoji cha Rwamisha aliyemtaja kwa jina moja la Kahatano.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment