Home » » BUKOBA MWENYEJI MKUTANO WA LAVLAC

BUKOBA MWENYEJI MKUTANO WA LAVLAC

 
Na Audax Mutiganz, Bukoba
HALMASHURI ya Manispaa ya Bukoba itakuwa mwenyeji wa mkutano wa 15 wa Ushirikiano wa Nchi za Afrika Mashariki (LAVLAC).

Kwa mujibu wa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Amani, mkutano huo utajumuisha halmashauri za wilaya na manispaa 130 zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Katika taaarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Amani alisema mkutano huo utafanyika katika viwanja vya Jimkana vilivyoko Manispaa ya Bukoba kuanzia keshokutwa Agosti 30 mwaka huu.

Mstahiki meya huyo alisema Tanzania itawakilishwa na halmashauri za wilaya na manispaa zipatazo 28 kutoka katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.

Alisema mkutano huo utaenda sambamba na maonyesho mbalimbali yanayozihusisha taasisi mbalimbali za kiserikali, mashirika ya umma na watu binafsi.

Amani alisema kauli mbiu ya mkutano huo itakuwa Serikali za Mitaa na Utatuzi wa Mabadiliko ya Tabia Nchi. Kwa mujibu wa Amani, maandalizi ya mkutano huo yameshakamilika.

Alisema Manispaa ya Bukoba imeomba Rais Jakaya Kikwete awe mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo na kwamba manispaa yake inasubiri jibu kutoka Ikulu.

Amani aliwataka wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kutokana na mkutano huo, kwa kufanya biashara ili waweze kujiongezea kipato kutokana na kuwepo kwa ugeni huo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa