Home » » KAMATI YA SENSA LAWAMANI

KAMATI YA SENSA LAWAMANI


na Mbeki Mbeki, Ngara
MAKARANI wa sensa 125 katika Kata ya Omurusagamba, wilayani Ngara, Kagera, wameilalamikia Kamati ya Sensa wilayani hapa kushindwa kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo litakalofanyika Agosti 26.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya makarani hao walisema, baada ya kumaliza mafunzo hayo yaliyochukua siku 11, wamekaa vituoni muda mrefu bila kukabidhiwa vifaa vya kufanyia kazi.
“Hii hali inatukatisha tamaa, fedha tuliyolipwa hakuna gharama ya kulala, hapa tunapoendelea kukaa tunaongezewa gharama zisizo za lazima,” alisema mmoja wa makarani hao.
Mmoja wa makarani hao, Mwalimu Privatusi Andrew, alisema uongozi wa wilaya haujatoa taarifa kwao kujua hatma ya vifaa hivyo na kutoa tahadhari kwa uongozi wa wilaya kuhakikisha vinatolewa kwa muda mwafaka.
Andrew alizitaja sehemu nyingine ambazo zimecheleweshewa vifaa vya sensa, ni Rulenge, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ilemera, Ngara Sekondari na Omurushagamba.
Pamoja na hayo, alisema makarani hao hawakupata fomu za mikataba wala kiapo cha kufanya kazi na kuongeza kuwa, mkataba uliopo una mapungufu kwani hautaji muda wa kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu, alisema makarani hao wamepewa ushirikiano wa kutosha na taratibu zote zinaendelea kama kawaida.
“Jukumu la kugawa vifaa ni letu, logistics zote zimepangwa vizuri, ninapozungumza na wewe magari yanazunguka kugawa vifaa,” alisema Kanyasu na kuwataka makarani hao kuwa wavumilivu muda wa kugawa vifaa bado upo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa