na Ashura Jumapili, Bukoba
WANANCHI wa Mkoa wa Kagera jana walisotea huduma ya usafiri kutokana na mgomo wa madereva waliokuwa wakiishinikiza Manispaa ya Bukoba kupunguza tozo ya ushuru wa stendi kuu ya mabasi.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema walishindwa kufanya shughuli zao mbalimbali kutokana na kukosa usafiri wa kuwapeleka maeneo tofauti.
Salehe Mashaka mkazi wa Kata ya Kamachumu Wilaya ya Muleba, alisema mgomo huo umewaathiri kwa kiasi kikubwa sambamba na kukwaza shughuli za kiuchumi na hivyo kuwaweka katika wakati mgumu.
Alisema kuwa kufuatia mgomo huo, nauli zilipandishwa mara tatu ya nauli za awali kutoka sh 2,000 hadi sh 10,000 kwa safari za Kamachumu-Bukoba mjini.
Naye Mariam Mlama mkazi wa Wilaya ya Karagwe, alisema mgomo huo ulimfanya ashindwe kusafiri kuelekea kwenye kituo chake cha kazi.
Alibainisha kuwa alipofika stendi kuu ya mabasi mjini Bukoba akiwa amefuatana na wenzake watatu, waliambiwa kuwa nauli ya kwenda Karagwe ni sh 15,000 badala ya sh 5,000 ambayo ni nauli halali.
Aliongeza kuwa pamoja na nauli hiyo kupanda, bado hakukuwa na mabasi ya kubeba abiria kituoni hapo hali iliyowalazimu kusubiria mabasi makubwa yanayotoka Mwanza kuelekea Karagwe yanaoyoingia mjini Bukoba saa tisa alasiri.
Mmoja wa madereva wa mabasi madogo yaendayo kwenye wilaya mbalimbali yakitokea mjini Bukoba, Abdallah Msakanjia, alisema wameamua kugoma ili kuishinikiza serikali ya mkoa huo kushughulikia malalamiko yao ya ushuru wa stendi.
Alisema basi dogo (Hiace), kila linapotoka stendi hulipia ushuru wa sh 2,000 bila kujali limebeba idadi gani ya watu wakati kituo hicho hakifanyiwi matengenezo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Khamis Kaputa, alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kutokana na kubanwa na majukumu ya serikali za mitaa kwenye miji iliyoko pembezoni mwa ziwa Victoria.
Kaputa alisema atakutana na wasafirishaji Septemba Mosi mwaka huu, kuzungumzia mgomo huo.
Chanzo: Tanzania Diama
0 comments:
Post a Comment