Home » » VODACOM YAPONGEZA MCHANGO WA VYOMBO VYA HABARI

VODACOM YAPONGEZA MCHANGO WA VYOMBO VYA HABARI

Na Mwandishi Wetu, Kagera
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imewashauri wadau wa masuala ya kilimo, kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika kutekeleza sera ya Kilimo Kwanza.

Akizungumza mjini hapa wakati wa kilele cha Maonyesho ya Kilimo ya Nanenane, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, alisema vyombo vya habari vinafanya kazi kubwa ya kuhabarisha na kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu masuala mbalimbali ya kilimo.

“Vyombo vya habari vinafanya kazi kubwa ya kutoa taarifa mbalimbali za kilimo na biashara. Kutekeleza sera ya Kilimo Kwanza vyombo hivi vinapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa ndio daraja kati ya wakulima, wafanya biashara na walaji.

“Sera ya Kilimo Kwanza ni nzuri na imepokelewa vizuri na mataifa mengi. Kuna umuhimu mkubwa vyombo vya habari vishirikishwe katika semina na makongamano na kupewa elimu kuhusu masuala ya kilimo,” alisema Meza.

Akizungumzia huduma mbalimbali ambazo kampuni hiyo inazitoa kwa wakulima na wadau wa kilimo, alisema Vodacom inaboresha zaidi huduma yake ya M Pesa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wakulima na wafanyabiashara.

“Sasa tunayo huduma ya M Pesa ambayo imerahisisha shughuli kati ya mkulima na mfanyabiashara. Sasa kupitia mawakala wetu zaidi ya elfu ishirini na tano nchini tumeondoa ulazima wa mkulima kusafiri kutoka kijijini kuleta mazao mjini. Kupitia huduma yetu sasa anaweza kupokea fedha kutoka kwa mfanyabiashara na yeye kutuma mazao kupitia njia za usafiri zilizopo na hii inaokoa muda na usumbufu kwa wakulima.

“Tutaendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali na wadau wa masuala ya kilimo kwa ajili ya kuleta mapinduzi katika sekta hii ambayo imeajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania na hatimaye kilimo kiwe na tija kwa wakulima na kukuza uchumi wa nchi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa