Home » » WENYEVITI WA MITAA BUKOBA WASUSIA SENSA

WENYEVITI WA MITAA BUKOBA WASUSIA SENSA

Na Renatha Kipaka, Bukoba
WENYEVITI wa Serikali za Mitaa katika Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, wamesema hawako tayari kutoa ushirikiano wakati wa kazi ya Sensa, kutokana na kutoshirikishwa kikamilifu na uongozi wa manispaa hiyo.

Akizungumza katika kikao chao cha kawaida cha wenyeviti wa mitaa, ambacho pia kilikuwa na ajenda ya kujadili ushiriki wa Sensa, Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti hao, Yusuph Mbagwa, alisema hadi sasa wanasikia wanatajwa tu kwenye vipeperushi, lakini hawajapewa maelezo yoyote na manispaa.

Alisema wenyeviti, wamekuwa wakiwekwa kando kipindi kirefu kwa kutoshirikishwa kikamilifu, yanapotokea mambo mbalimbali ya kitaifa.

“Sisi ndio tunatambua wananchi wanaohesabiwa walipo, lakini tunatajwa tu kwenye vipeperushi na vyombo vya habari kuwa tutahusika kuwaongoza wahesabuji, tutawaongoza vipi bila kupewa semina na kujua manispaa itatujali vipi, maana sisi hatulipwi mshahara na Serikali tunafanya kazi za kujitegemea,” alisema.

Alisema siku ya Sensa, watakaa nyumbani na familia zao ili wahesabiwe kama watu wengine, kwani hawawezi kuzunguka na makarani mitaani.

Akijibu ma malalamiko hayo, Mratibu wa Sensa Manispaa ya Bukoba, Alphonce Mwakabesa, alisema bajeti iliyotengwa na ofisi ya Takwimu ya Taifa, haikujumuisha wenyeviti wa mitaa.

Alisema waliowekwa kwenye bajeti hiyo, ni watendaji wa kata na watendaji wa mitaa.

Alisema hadi sasa, Manispaa ya Bukoba imepokea Sh milioni 103, kwa ajili ya mafunzo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa