Home » » NG’OMBE 25 WAUAWA KWA RISASI

NG’OMBE 25 WAUAWA KWA RISASI


na Victor Eliud, Muleba
ASKARI wa Kikosi cha Kudhibiti Ujangili katika mapori ya akiba ya Buligi, Kimisi na Biharamulo mkoani Kagera, wanadaiwa kuua kwa risasi zaidi ya ng’ombe 25 wanaomilikiwa na wafugaji wilayani Muleba.
Tukio hilo limetokea Jumanne wiki hii katika pori la akiba la Kimisi baada ya askari hao kuwakuta ng’ombe hao wakipata malisho.
Kufuatia mauaji hayo ya kinyama, baadhi ya wafugaji na wamiliki wa mifugo katika Wilaya ya Muleba wamewalalamikia askari hao na kumtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamisi Kagasheki kuingilia kati sakata hilo ili kunusuru mifugo yao kuuawa kinyume na sheria.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafugaji hao; Mnana Kalela na Elias Saba wamewatuhumu baadhi ya askari wa kikosi cha kudhibiti ujangili kwenye mapori hayo kutokana na kuomba rushwa ili kuiachia mifugo yao.
“Mimi kilichonishangaza ni pale askari hao walipoamua kuwapiga risasi ng’ombe wetu…inamaana waliokuwa wamevunja sheria ni ng’ombe au wamiliki wa mifugo hiyo? Kilichotakiwa hapo ni kutukamata sisi wamiliki badala ya kupiga risasi ng’ombe zetu,” alisema Kalela.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kihindo, Kijiji cha Bihata wilayani Muleba, Medard Polcup amelaani vikali mauaji ya ng’ombe hao kutokana na askari wa wanyama pori kulazimisha kupewa rushwa ya sh milioni 10 kinyume na sheria.
Amedai kuwa baada ya mifugo hiyo kuuawa kwa risasi, wamiliki wake wamelazimika kuwagawia nyama wananchi wanaoishi kwenye Kijiji cha Kihindo jirani kabisa na pori la hifadhi la Kimisi na kwamba hatua hiyo imewasababishia umaskini mkubwa.
Meneja wa mapori ya akiba ya Buligi, Biharamulo na Kimisi, Henock Msocha alipotakiwa kujibu tuhuma dhidi ya askari wa kikosi hicho kujihusisha na vitendo vya kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa wafugaji, alikanusha vikali huku akikiri kuuawa ng’ombe 25 na kuwajeruhi wengine nane baada ya kukutwa wakiwa ndani ya pori la akiba kinyume na sheria.
“Ki ukweli ndugu mwandishi ng’ombe hao tuliwaua…na hii ilitokana na mifugo hiyo kukutwa ndani ya hifadhi kinyume na sheria…lakini jambo la askari wangu kwamba waliomba rushwa sikubaliani nalo…isitoshe wahalifu wengi hupenda kusingizia maneno kama hayo ili kuzorotesha jitihada za serikali katika kudhibiti uhalifu wanaoufanya,” alisema Msocha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi alikiri kuwepo kwa tukio hilo, ingawa suala la askari hao kuomba rushwa alidai kutokuwa na taarifa nalo, na kuelekeza kwamba iwapo kuna malalamiko kama hayo jeshi lake litafanya uchunguzi ili kubaini ukweli kabla ya kuchukua hatua.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Masawe alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo, ni kuwa wamiliki wa mifugo hiyo walikuwa wakipambana kwa risasi na askari wa wanyama pori na kwamba baada ya kujificha kwenye mifugo hiyo baadhi ya risasi ziliwapiga ng’ombe hao na kusababisha vifo.
Alisema serikali ya mkoa tayari imeshatoa maelekezo kwa viongozi wa kata na vijiji kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wakulima na wafugaji ili kuondoa uvunjifu wa amani unaoweza kujitokeza.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa