Home » » KAGERA YAHITAJI MAMILIONI KULINDA MIPAKA YA NCHI

KAGERA YAHITAJI MAMILIONI KULINDA MIPAKA YA NCHI

Mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe

Mkoa wa Kagera unahitaji Sh. milioni 400 ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoukabili maeneo ya mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani zilizo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mkuu wa mkoa huo, Kanali mstaafu Fabian Massawe, alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya mkoa huo kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Kanali Massawe alisema maeneo ya mipaka ya Tanzania na nchi za Rwanda, Burundi na Kenya (upande wa Ziwa Viktoria) inakabiliwa na changamoto nyingi zinazotokana na ukosefu wa rasilimali hasa fedha, ili kukabiliana navyo.

Alisema eneo hilo ambalo kwa sehemu kubwa ni msitu, linahitaji ushiriki wa taasisi zinazounda kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo, kufanikisha jitihada za kukabiliana na changamoto hizo.

Hata hivyo, Kanali Massawe alisema sehemu ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini, wanakaribishwa na wenyeji ili kushirikishwa shughili za uzalishaji kama kilimo, uvuvi na kuchunga mifugo.

Kwa mujibu wa Kanali Massawe, takwimu rasmi inayohusisha watu walioorodheshwa inaonyesha kuwepo wahamiaji haramu 35,000 mkoani Kagera.

Alisema ongezeko la wahamiaji haramu linaweza kuibua machafuko kama inavyotokea hivi sasa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Alisema wahamiaji haramu kutoka nchi tofauti waliingia mashairiki ya DRC na kufanikiwa kuweka makazi ya kudumu, sasa wamekuwa chanzo cha migogoro nchini humo.

Hata hivyo, Sitta alielezea kushangazwa kwake na taarifa za kuhitajika kwa fedha hizo (Shilingi milioni 400) kwa vile serikali ilishaidhinisha zitolewe.

Akijibu baadhi ya hoja za Kanali Massawe, Sitta alisema mikoa iliyopo maeneo ya mipakani kama Kagera, inahitaji uwekezaji na uwezeshaji ili kukabiliana na changamoto ikiwemo ya kukabiliana na wahamiaji haramu.

Pia Sitta alisema ipo ya haja kwa Wakuu wa Wilaya za mpakani kuwasiliana na nchi jirani ili kuunda kamati za ujirani mwema hadi ngazi za vijiji, ili kurahisisha mwingiliano hasa unaohusu utafutaji wa mahitaji ya kibinadamu.

Alitoa mfano wa baadhi ya maeneo mkoani Kilimanjaro na Arusha yanayopakana na Kenya, serikali za vijiji zinatoa vibali vya aina hiyo, vikilenga kufika eneo lisolozidi kilomita 30 kutoka mpakani.

Akiwa katika mpaka wa Mutukula unaozitenganisha Tanzania na Uganda, Sitta alipiga marufuku vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wafanyabiashara wadogo aliowaita kuwa wajasiriamali.

Amri hiyo ilifuatilia swali aliloulizwa na mmoja wa wafanyabiashara hao, Sauda Athumani, akielezea kunyanyaswa kwao na halmashauri ya wilaya ya Missenyi kupitia kwa mzabuni wa ukusanyaji ushuru waliomtaja kwa jina moja la Kimela.
Chanzo: Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa