na Mbeki Mbeki, Karagwe
KAMATI ya Sensa wilayani Karagwe mkoani hapa, imepitisha majina 1,388 yatakayohusika na zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 26.
Hayo yalisemwa jana na mratibu wa sensa wilayani Karagwe, Moris Mulilo katika kikao cha kupokea majina ya makarani wa sensa kilichofanyika ofisini kwa mkuu wa wilaya.
Mulilo aliyasoma majina ya makarani hao kwa Kamati ya Sensa ambapo iliyathibitisha na kukubaliana na utaratibu uliotumika wa kila mshiriki kutuma maombi na kwa kuzingatia sifa zao.
Alisema kuwa, makarani wa dodoso fupi ni 803, dodoso refu ni 460, wasimamizi ni 103 na 22 watakuwa ni makarani wa tahadhari ambapo aliongeza kuwa semina yao itaanza rasmi leo.
Mratibu huyo alisema, ili kurahisisha kazi ya kuhesabu watu, wilaya yake imetengwa katika maeneo madogo madogo katika mfumo wa taarifa za kijiografia na kuwa kila eneo lililotengwa limechorwa ramani inayoonesha mahali lilipo pamoja na mipaka yake.
Aliongeza kuwa, utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu, umefanywa katika eneo la wilaya ikiwa ni pamoja na maeneo ya makazi ya watu, visiwa, misitu, mbuga za wanyama na maeneo ya wafugaji.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo viongozi wake wanapaswa kuhamasisha watu wao kushiriki zoezi hilo, ni Kafunjo, Bitaraka, Kahundwe, Nyakasimbi, Bigoro, Rushosho na Omukakanja kutokana na jiografia ya maeneo husika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya, Darry Rwegasira alisema kuwa uhamasishaji wa wananchi na wadau wengine kushiriki katika kufanikisha sensa, umeanza muda mrefu katika wilaya yake, na kuongeza kuwa kadiri muda unavyokaribia, ndivyo shughuli za uhamasishaji zinavyoimarishwa.
Rwegasira ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Wilaya, alisema kamati hiyo ina jukumu la kusimamia zoezi hilo katika maeneo yao, kutoa ushauri wa utekelezaji na kuandaa umma kwa kuwaelimisha wananchi pamoja na matarajio ya ushiriki wao katika zoezi hilo muhimu kitaifa.
Aidha, alisema kuwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inafanyika kwa mujibu wa sheria ya takwimu Na. 1 ya mwaka 2002, ambapo kutokana na sheria hiyo, taarifa zote binafsi za watu zitakazokusanywa wakati wa zoezi hilo ni siri na zitatumika kwa madhumuni ya kitakwimu.
Hata hivyo, watu wote watakaohusika na kazi ya kuhesabu watu, watalazimika kula kiapo cha kutunza siri ya taarifa binafsi za watu watakaowahesabu kabla ya kuanza kazi hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment